Matonya ‘NO’ Makundi ‘NO’ Mashabiki Mitandaoni

NI mshindi wa tuzo nane za Kilimanjaro, ana miliki Tuzo ya Kisima kutoka Kenya, amefanya albamu nne tangu adumu kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva ambazo ni Siamini, Umoja ni Nguvu, Safari ya Dunia na Dunia Mapito.
Wimbo uliomtambulisha vyema kwenye gemu unaitwa Vailet, lakini alikimbiza pia kwa ngoma kadhaa ikiwemo Anita, Siamini, Taxi Bubu, Dunia Mapito na nyingine nyingi.
Miongoni mwa kolabo zake bora ni Wimbo wa Anita aliofanya na Lady Jaydee au ikipenda unaweza kumuita Komando, Usinikubali Haraka alioshirikishwa na Fid Q, Ukweli wa Moyo wa Nay wa Mitego na Wimbo wa Angwelina aliojumuika pamoja na Christian Bella.

Bila shaka umeshafahamu ninamzungumzia nani! Kama hujanusa chochote; aaah! Namzungumzia ‘legendary’ kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva, Seif Shabani ‘Tonya Mbili’, ambaye kwa sasa wimbo wake wa hivi karibuni wa Kiherehere unafanya vizuri.
Matonya ana mengi amezungumza kwenye mahojiano na Mikito NusuNusu, ni mahojiano matamu ndiyo maana yanaletwa hapa ili yachangamshe akili zako msomaji na kuzifanya siku ziende ‘smooth’ kabisa. TWENZETU BASI.

MIKITO: Kwanza kabisa unazungumziaje gemu la Bongo Fleva kwa sasa, kama mkongwe ni changamoto gani unakutana nazo kutokana na kasi ya muziki inavyokwenda?
MATONYA: Ninachoweza kusema ni kwamba changamoto ya jana ni tofauti na ya leo na changamoto ya leo ni tofauti na ya kesho. Kwa hiyo kwa namna yoyote mambo yanavyobadilika sina budi kubadilika nayo ndiyo maana unaona mpaka leo bado niko fiti kwenye gemu.
MIKITO: Kuna projekti yako yoyote ambayo unaweza kuizungumzia kwa sasa tukawafahamisha mashabiki wako?

MATONYA: Projekti ni nyingi kiukweli na Mungu akijalia, baada ya Mfungo wa Ramadhan tutazindua dtudio inayoitwa Bizznenga Music ambayo itakuwa chini ya Prodyuza Kimambo Touchers na wenzake kadhaa.
Katika kuseti mitambo ya studio hiyo mpya nimefanya jaribio kwa kufanya ngoma kadhaa kali ikiwemo ya Kiherehere ambayo kwa sasa ni gumzo mitaani.
MIKITO: Wanamuziki wengi wanadaiwa kutumia kiki kusukuma kazi zao, unafikiri hili linaupeleka wapi muziki na nini maoni yako?
MATONYA: Kiukweli, mimi naona kama kuna chochote kile kinaweza kufanywa na kuingiza pesa hata kwa njia ya kucheza na akili za watu, sioni kama ni jambo baya, watu waendelee tu kufanya ikiwa ni pamoja na kufanya muziki mzuri.
MIKITO: Kwa wanamuziki waliyopo kwenye gemu kwa sasa unamkubali nani?

MATONYA: Bahati nzuri ni kwamba wengi ambao wanafanya vizuri nipo nao karibu, kwa hiyo ninawakubali wengi na ninafanya kazi na wengi kwa sababu tunajenga nyumba moja. Ingawa kwa sasa naona kuna matabaka yameanza kuibuka kwenye gemu.
MIKITO: Matabaka gani hayo unazungumzia?
MATONYA: Makundi na timu zisizokuwa na maana. Sisemi kuwa na makundi ni jambo baya lakini kuwa nayo kwa lengo la kumbomoa msanii mwingine ni jambo nisilolipenda hata kidogo.
MIKITO: Kwenye Wimbo wa Kiherehere umeweka wazi mwenyewe kwamba kuna stori mtaani unahusishwa na biashara ya unga, unafikiri kwa nini unahusishwa?

MATONYA: Nimefanya mengi kwa mashabiki tangu muda ambao nimekaa kwenye gemu, ninamuomba Mungu nifanye mengi zaidi. Kuna mengi mazuri na mabaya naomba nisamehewe kwani pia ni mwanadamu. Lakini nimefanya mengi…mengi…mengi…!
MIKITO: Hujaniweka wazi kuhusu tuhuma za unga, naona kama umekwepakwepa kiana.
MATONYA: Naomba uelewe jibu langu, nimesema kama kuna kosa jamii mnisamehe tu, sina zaidi ya hilo.
MIKITO: Vipi kuhusu kipato chako kwenye muziki, unakipata zaidi kupitia kazi gani hasa?
MATONYA: Nashukuru kipato kinaimarika siku hadi siku. Kwenye shoo, kuuza nyimbo na mambo mengi yanayotokana na muziki huu ninaoufanya. Kilichopungua ni kuuza tu albamu kwa Wahindi, lakini mikakati ipo ya kuongeza soko zaidi.
MIKITO: Mpaka sasa kwa muda ambao umekaa kwenye gemu unajivunia nini hasa?
MATONYA: Ni utajiri nilioupata. Nimekaa kwenye gemu kwa muda mrefu na kiukweli nimeweza kupata utajiri wa rasilimali watu, hicho ni kitu ambacho ninajivunia sana kiukweli.

MIKITO: Views za YouTube, ni baadhi ya vitu vinavyowafanya wanamuziki wengi kwa sasa kuwa ‘busy’ na kuanzisha timu kwenye mitandao ya kijamii, kwako hili limekaaje?
MATONYA: Muziki mzuri unajipromote wenyewe, ukifanya kazi nzuri na kuisukuma itafika mbali, bila hata kuweka timu na mambo mengine.
MIKITO: Unaona ni jambo gani ambalo halijakaa poa kwenye gemu?
MATONYA: Ambacho hakipo sawa tulikiona toka muda mrefu. Ni juu ya umoja, hakuna umoja thabiti kwenye gemu. Baada ya watu kuona kwamba muziki ni mchanga wenye dhahabu wamekuwa wakigeukana, hicho ndicho ninaweza kusema, lakini umoja ni muhimu sana.

MIKITO: Kila video unayotoa ni kali, nini siri ya hili ikoje?
MATONYA: Matonya ni mtu ambaye anapenda kufanya kazi bora, kuhusu ‘madairekta’ Bongo wanafanya kazi nzuri kiukweli. Namkubali Travellah, Pabro aliyenifanyia ngoma ya Zilipendwa na hata Hanscana yupo poa sana!
MIKITO: Tumeona wakongwe wanaoa, vipi kwa upande wako, mpango huyo upo?

MATONYA: Hiyo ni sehemu nyeti sana na itazidi kuwa nyeti siku zote. Kwangu ni sehemu muhimu, kwani nafahamu nikiharibu huko nimeharibu maisha yangu yote. Lakini Matonya ana mtu ambaye anampenda, pia ana watoto. Mungu akipenda kulifanya jambo hili siku moja kwa namna moja au nyingine liwe basi ‘inshallah’, itakuwa.
MIKITO: Asante sana Matonya, pengine jambo la mwisho kwa mashabiki wako.
MATONYA: Nawapenda sana na tuzidi kushirikiana tu kwenye kazi.