RAMMY GALIS, Mambo Gani Hayo Unatuletea?

ILIKUWA ni sekunde, dakika, siku na sasa ni wiki kadhaa tangu mwanadada Agnes Gerlad ‘Masogange’ atutoke, tunazidi kukuombea kwa Mungu akupunguzie adhabu za kaburi na kuipumzisha pema roho yako, mbele yako, nyuma yetu.
Sipendi sana kukum­bushia habari za msiba kwa sababu najua wapo watu ambao wanaumizwa sana na kilichotokea, lakini kazi ya Mungu haina makosa na ni vizuri tuliobaki tukapata nafasi ya kujifunza.
Miongoni mwa matukio yaliyotokea katika msiba wa Masogange, wakati mwili wake ukiagwa pale Leaders Club, ni tukio la aliyekuwa mpenzi wake, Rammy Gallis ‘kuzimia’ na kusababisha mjadala mzito uibuke kuhusu tukio hilo, wengi wakielezea kwamba jamaa aliamua kutafuta kiki kwenye msiba wa Ma­sogange.
 
‘Uzimiaji’ wa Rammy ndiyo ulioleta gumzo kubwa kwani alionekana akiwa ameshikilia kitambaa chake cha mkononi vizuri kama mtu anayejitambua, huku miwani yake ikiwa machoni, tofauti na vile mtu aliyezim­ia anavyotegemewa kuwa.
Mwanadada Irene Paul ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipeleka ishu hiyo kwenye mitandao ya kijamii,
ambapo aliposti ujumbe akimshutumu Rammy kwa kutafuta kiki msibani, huo ukawa mwanzo wa kutupi­ana maneno kati ya wasanii hao wawili.
Mengi yalizungumza na kwa bahati nzuri nilipata bahati ya kuzisikiliza pande zote mbili na kulitazama tukio hilo kwa jicho la tatu.
 
Ukimsikiliza Rammy, maelezo yake yanajitoshele­za vizuri kwamba hakuzimia bali aliishiwa nguvu, jambo ambalo ni la kawaida sana hasa kama umefanya kazi nyingi zinazokulazimu kusimama muda mrefu au kutumia nguvu nyingi.
Maelezo hayo yalikuwa yametosha kabisa kumaliza utata wote uliotokea kwa sababu ni kweli inawezeka­na kabisa ukaishiwa nguvu na kubebwa lakini ukaweza kushikilia si tu kitambaa, hasa simu na isidondoke.
 
Hata hivyo, maneno mengi yasiyo na msingi, zikiwemo kashfa ali­zoanza kuziibua Rammy kwenda kwa Irene Paul, yaliwashangaza wengi na kuwafanya hata ambao walishalichukulia poa tukio hilo waanze kufuatilia kwa kina kujua ni nini hasa kili­chokuwa kimetokea.
Rammy amesikika akim­tuhumu mambo chungu nzima, kwamba anagom­bana na wasanii wenzake hovyo wawapo location, akaenda mbali zaidi na kusema kwamba Irene ana matatizo ya akili.
 
Sina lengo la kumtetea mtu yeyote katika hili lakini ukisikiliza majibu aliyoya­toa Irene wakati akifanya mahojiano na kituo kimoja cha runinga, utaona ni kwa namna gani amekomaa kiakili na kisanii. Narudia tena, ilitosha kabisa kwa Rammy kuishia kwenye majibu yake ya msingi kwamba hakuwa amepoteza fahamu bali aliishiwa nguvu, full stop.
Ukifuatilia kwa kina, utagun­dua kwamba si Irene pekee aliyekuwa akimtuhumu Rammy kupanga na kutekeleza kiki kwenye msiba wa mwenzake. Inaonesha watu walikuwa wanajua na wapo waliomsaidia kutimiza kiki hiyo. Mfuatilie vizuri Idriss Sultan ambaye siku hiyo alikuwa ‘beneti’ na Rammy na hata alipoanguka alikuwa miongoni mwa watu waliomsaidia.
 
Uso wa Idriss katika tukio hilo, ulikuwa ukizungumza lugha tofauti kabisa, na hata picha aliyoposti baadaye kwenye akaunti yake ya mtandao wa In­stagram, inadhihirisha kwamba alikuwa anajua kinachoende­lea.
Kitendo cha wewe kuto­kwa na mapovu kiasi hicho, kinamaanisha kweli ulikuwa umejipanga kutengeneza kiki, utasemaje kwamba siku hiyo ilikuwa ‘siku yako’ wakati unajua fika kwamba mpaka Masogange anafikwa na mauti alikuwa ameshaachana na wewe kitambo na alikuwa na maisha yake mengine?
 
Unataka kusema siku hiyo wewe ulikuwa na umuhimu kuliko binti yake? Unataka kusema wewe ulikuwa na umuhimu kuliko baba mtoto wake au kuliko mwanaume aliyekuwa akiishi naye na ndugu zake wengine?
Mantiki ya kuleta drama wakati wa kuaga na baada ya hapo ni nini? Umekosa utu ki­asi gani mpaka ufanye mzaha kwenye tukio la huzuni kama kifo? Usanii wa kutegemea kiki ni ushamba kama ulivyo ushamba mwingine wowote. Watch your back buddy!