Hivi Ndivyo Zali Alivyozima Mbwebwe za Daimond

Hivi Ndivyo Zali Alivyozima Mbwebwe za Daimond
Dunia inakwenda spidi sana! Miezi kadhaa baada ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumwagwa na mama watoto wake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, bado mambo ni moto huku mwanamama huyo akidaiwa kuzima ngebe au mbwembwe za jamaa huyo, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.

Wakati Diamond akibadili rangi ya lile gari lake aina ya BMW X6 kutoka nyeusi kwenda bluu bahari, Zari yeye alijibu mapigo kwa kununua gari la kifahari aina ya Range Rover Spot lenye rangi nyeupe na kuibua gumzo kubwa kwa mashabiki wao.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, Diamond aliamua kulibadili gari hilo rangi kwani lilikuwa limezoeleka mitaani jijini Dar tangu alipopewa kama zawadi siku ya bethidei yake mwaka 2014 alipokuwa akitimiza umri wa miaka 25. Mbali na kubadili rangi ya gari hiyo, pia alibadilisha ‘rim’ za matairi yake na kuweka nyingine kali zaidi ya zile za awali.
Watu walioko karibu na Zari walidokeza kuwa, mfanyabiashara huyo alivuta ndinga hilo wikiendi iliyopita na kuthibitisha kwamba, yeye ni Boss Lady wa ukweli ambaye anaweza kufanya makubwa hata bila kuwa na mwanaume, tofauti na wengi walivyodhani kwamba kummwaga Diamond ndiyo utakuwa mwisho wake. Vyanzo vilikwenda mbali zaidi na kutaja thamani ya gari hilo la Zari kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 171 huku lile la Diamond likiwa na thamani ya shilingi milioni 150.

Zari alitangaza mpango wake wa kununua gari hilo wiki chache zilizopita na hatimaye wikiendi hii alilianika gari hilo jipya na kuliweka kwenye mitandao ya kijamii. Zari alitimiza azma yake hiyo kama alivyoahidi mapema mwaka huu kwamba, kuna mambo alipanga kuyafanya ndani ya Mwaka 2018 ikiwemo kulimiliki gari hilo.

Hata hivyo, mara baada ya kuliweka gari hilo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuandika; ‘Come through baby girl’, baadhi ya watu walidai kwamba, gari hilo amenunuliwa na mwanaume wake mpya ambaye ni mfanyabiashara maarufu jijini Dar (uchunguzi wetu ukikamilika tutamwanika).

Kufuatia madai hayo, Zari alikanusha kupitia ukurasa wake wa Snapchat ambapo aliweka wazi kuwa amelinunua kwa fedha zake mwenyewe. Mbali na gari hilo, mwaka huu, Zari pia aliahidi kuanzisha migahawa mikubwa kama KFC au McDonalds.

Ili kusikia maoni yake juu ya kufuru za Zari ambazo zimelenga kumkata ngebe, katika harakati za kumsaka Diamond gazeti hili lilifika kwenye ofisi mpya za Wasafi zilizopo Kwazena, Mbezi-Beach ambapo lilijuzwa kuwa jamaa huyo alikuwa nchini Uingereza kikazi.

Alipotafutwa kwa njia ya WhatsApp, Diamond hakujibu ‘chatting’ hivyo jitihada zinaendelea ili kupata maoni yake. Hata hivyo, mmoja wa watu waliokutwa ofisini kwake alisema hawezi kuzungumzia masuala binafsi badala yake aulizwe mambo ya kazi yake ya muziki.

Zari, mbali na gari hilo, pia alishaanika umiliki wake wa magari ya kifahari kama Mercedez Benz, Audi, Hammer, Ferrari na mengineyo huku Diamond akimiliki magari mengine kama Toyota Prado, Toyota Land Cruiser V8 na mengine madogomadogo.