Joshua, Wilder watishiana bei kuvunja rekodi ya masumbwi
Bingwa wa dunia wa masumbwi wa uzito wa juu, Anthony Joshua amesema yuko tayari kupambana na bingwa mwenzake ambaye hajawahi kupoteza pambano, Deontay Wilder ili kumpata bingwa wa kiwango cha juu zaidi yaani ‘undisputed. 

Joshua ambaye alitegemewa kupambana na Alexander Povetkin baada ya kumshinda kwa pointi Joseph Parker, amesema kuwa anataka kukata mzizi wa fitna kati yake na mbabe huyo na kwamba tayari wameshaitumia timu ya Wilder ofa ya pambano. 

Kwa mujibu wa promota wa Joshua ambaye anaandaa pambano hilo nchini Uingereza, wameitumia timu ya Wilder ofa ya $ 12.5 milioni lakini timu hiyo imeikataa. 

Timu ya Wilder imetaka kuwe na mgawanyo wa asilimia 60-40, wakidai kuwa pambano hilo linaweza kuingiza zaidi ya $100 milioni, hivyo wanataka $40 milioni.