Rah P, Asihesabu Makosa Yake, Aangalie Ni Hatua Gani Asaidiwe Kuchukua Ili Makosa Yasijirudie


Ukizungumzia miongoni mwa marapa wa kike waliokuwa wanachangamsha gemu ya Bongo Fleva kwa miaka ya nyuma basi huwezi kuacha kumtaja Rah P ambaye alitamba na kibao chake cha ‘Hayakuhusu’.

Rah P ambaye jina lake halisi ni Fredinah Peyton alizaliwa Mwanza Juni 28, 1986 na kusoma mkoa humo hadi kidato cha sita, lakini muda wote huo mzuka wa HipHop ukawa umeshamshika japo wazazi wake hawakupendelea afanye shughuli hiyo. 

Upenzi huo wa fani ya muziki ulimwezesha kupata kazi ya kuendesha kipindi cha ‘African Beat’ katika Radio ya Kiss FM

Mwaka 2004 Januari ndipo alipoingia Bongo Records ikiwa chini ya producer P Funk na kurekodi kibao kilichompa sifa cha ‘Hayakuhusu’. Wakati wa utengenezaji wa video ya wimbo huu, minong’ono ya Rah P kuwa na uhusiano na Mwisho Mwampamba ikaenea, wakati huo Mwisho alikuwa katika mahusiano na Ray C.

Rah P kila mara alikuwa akieleza kuwa walikuwa ni marafiki wa kawaida tu na hata Ray C alilijua hilo.

Baadhi ya nyimbo alizozitoa wakati huo zilikuwa ni Ma Fans, Loony Love na Boys. Kwa muda mwingi alikuwa akifanya shoo zake Uganda maana hata kusoma aliwahi kusoma huko.

Rah P alifanya uamuzi wa kuondoka nchini na kuelekea Marekani kujaribu  kutimiza ndoto yake ya kuwa rapper mkubwa. Alipofika huko mambo hayakuwa kama alivyopanga, alianza shule lakini msaada wa kifedha kutoka nyumbani haukuweko, hivyo katika kuzunguka akakutana na mwanamme waliyependana, ambaye alimuahidi angemlipia kukamilisha shule.

Hata hivyo, akajikuta amekwishazaa mtoto wa kwanza na mtu huyo. Hivyo hakukuwa tena na suala la shule, kwani mtu huyo akaanza kumnyanyasa, hatimaye akazaa mtoto wa pili na mtu huyo huyo ambaye baadaye alikamatwa kwani alikuwa msambazaji wa madawa ya kulevya, matokeo yake Rah P akajikuta peke yake na watoto katika nchi ambayo sheria ilikuwa haimruhusu kufanya kazi.

Lengo la makala hii ni kumkumbuka Rah P ili popote alipo ainuke na kuangalia mbele kwa kujiamini, asiangalie nyuma kwa majuto kwani muda bado upo na uzuri wa kipaji ni kwamba kinaishi milele.

Afahamu pia kwamba jamii ya mashabiki wa Bongo Fleva bado wanamtaka arejee katika ulingo wa muziki huo kwani wapenzi wake bado wanamkumbuka kutokana na burudani aliyokuwa akiwapa.

Rapa huyo alishajitengenezea kundi kubwa la mashabiki nikiwemo mimi mwenyewe Omary, kwa kweli nimemmisi na natamani kumsikia tena.

Binadamu yeyote ni lazima apitie kwenye majaribu ambayo kwa kiasi flani yanampa somo na kumtia hasira ya kutaka kuyashinda ili aendelee mbele kwani maisha ni kuishi na kujifunza.

Rah P anatakiwa asiangalie ni kwa kiasi gani amekosea bali ni kwa njia gani anaweza kurekebisha makosa yake ili yasijirudie tena.

Ujumbe kwa mwanamuziki huyo ni huu: Jina lako bado linaishi akilini mwa watu, wapo wasanii wengi waliowahi kuanguka na kuinuka tena kwa kishindo hivyo jifunze kitu kupitia Ray C.

Baada ya kusoma makala hii ni matumaini yangu utapata nguvu na utarudi tena kwenye gemu kuja kupambana na marapa wa kike wa sasa kama Chemical, Rosa Lee, Pink na wengine wengi.

Imeandikwa Na: Omary Ramsey